Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge - Amehitimisha kwa kutoa wito kwa Watanzania wote kutumia sikukuu za kidini kama nyakati za kutafakari, kuimarisha mahusiano ya kijamii, na kuendeleza utamaduni wa amani na upendo unaolinda umoja wa Taifa.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Leo tarehe 24-12-2025, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC) Atoa Salamu za Krismas kwa Wakristo.

Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemedi Jalala Mwakindenge, ametoa salamu za heri ya Sikukuu ya Krismas kwa Wakristo wote nchini Tanzania, kufuatia maadhimisho ya sikukuu hiyo yanayofanyika kesho, tarehe 25 Desemba 2025.

Katika ujumbe wake wa Krismas, Sheikh Jalala amewatakia Wakristo sikukuu njema iliyojaa amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, akisisitiza umuhimu wa sikukuu hiyo kuwa chachu ya kuimarisha maadili mema katika jamii.
Sheikh Jalala amesema kuwa Krismas ya mwaka huu iwe fursa maalum ya kuwaasa vijana wa Kitanzania kutambua wajibu wao kwa taifa, kuipenda nchi yao, na kuwa wazalendo wa kweli kwa kushiriki katika ujenzi wa amani, mshikamano na maendeleo ya Taifa.

“Krismas ya mwaka huu iwe ni sababu ya kuwaasa vijana kutambua umuhimu wa nchi yao na kuwa wazalendo, na iwe pia sababu ya Watanzania kuvumiliana, kuishi kwa amani na upendo bila kujali tofauti za kidini,” amesema Sheikh Jalala.
Ameongeza kuwa amani ya kweli hujengwa kwa kuheshimiana, kuvumiliana na kushirikiana miongoni mwa waumini wa dini tofauti, jambo ambalo limekuwa ni alama ya kudumu ya jamii ya Kitanzania.

Wakati huohuo, Mshauri wa Sheikh Mkuu wa TIC, Mzee Azim Dewji, amesema kuwa Krismas ya mwaka huu inapaswa kutumika kama jukwaa la kutoa mafunzo ya maadili kwa vijana na jamii kwa ujumla.
Mzee Dewji amebainisha kuwa miongoni mwa majukumu makuu ya taasisi za dini ni kutoa mwongozo wa kimaadili, kukuza tabia njema na kujenga jamii yenye hofu ya Mungu, mshikamano na uwajibikaji.
“Taasisi za dini zina wajibu mkubwa wa kutoa mafunzo ya maadili mema kwa wananchi, hususan vijana, ili kujenga jamii yenye misingi imara ya maadili, amani na mshikamano wa kitaifa,” amesema Mzee Dewji.

Amehitimisha kwa kutoa wito kwa Watanzania wote kutumia sikukuu za kidini kama nyakati za kutafakari, kuimarisha mahusiano ya kijamii, na kuendeleza utamaduni wa amani na upendo unaolinda umoja wa Taifa.

Your Comment